Mhe.
Asha-Rose Migiro ( Mb) Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba,
akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu mchango wa haki za binadamu na
utawala wa sheria katika kuunga mkono juhudi za kitaifa na kimataifa
kuelekea upunguzaji wa umaskini na maendeleo endelevu. Waziri Migiro
alikuwa miongoni mwa wanajopo wanne walioalikwa na Rais wa Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa kuhudhuria na kubadilishana mawazo kuhusu nafasi ya
haki za binadamu na utawala wa sheria katika ajenda za maendeleo
endelevu baada ya 2015. Pamoja na kuzungumzia masuala ya haki za
binadamu na utawala bora. Mhe. Waziri alisema Tanzania kupitia Rais wake
wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilianza kutekeleza mipango
ya maendeleo ikiwamo ya kupiga vita umaskini, magonjwa na elimu kwa
wote, malengo ambayo baadaye Jumuiya ya Kimataifa ilikuja kuyaita
Malengo ya Maendeleo ya Millenia MDGs.
Naibu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson akifungua majadiliano
kuhusu mchango wa haki za binadamu na utawala wa sheria katika kuunga
mkono juhudi za kitaifa na kimataifa na nafasi yake katika suala zima la
maendeleo endelevu baada ya 2015. Naibu Katibu Mkuu alimtambulisha
Waziri Migiro kama mtangulizi wake na katika hotuba yake alinukuu baadhi
ya maneno ambayo Mhe. Migiro aliwahi kuyazungumza kuhusiana na masuala
ya utawala wa sheria wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa.
Muwakilishi
wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa
Balozi Tuvako Manongi,akifuatilia majadiliano kuhusu mchango wa haki za
binadamu na utawala bora katika kusukuma mbele suala zima la upunguzaji
wa umaskini na maendeleo endelevu. Wachagizaji wakuu wa majadiliano hayo
alikuwa ni Mhe. Asha-Rose Migiro ( Mb) Waziri wa Sheria na Masuala ya
Katiba, Bw. Christoph Strasser, Bw. Nicolas Lusian na Bw. Martin
Kreutner.
Sehemu
ya washiriki wa majadiliano kuhusu mchango wa haki za binadamu na
utawala bora katika kuunga mkono juhudi za kitaifa na kimataifa kuelekea
upunguzaji wa umaskini na maendeleo endelevu wakimsikiliza Waziri wa
Sheria na Masuala ya Katiba Mhe. Asha-Rose Migiro ( Mb).
Na Mwandishi Maalum, New York
Waziri
wa Sheria na Masuala ya Katiba, Asha-Rose Migiro ( Mb) amesema,
ajenda za maendeleo endelevu baada ya 2015 zijielekeze zaidi katika
kuyawezesha makundi ya jamii yaliyo katika mazingira magumu.
Ameyasema
hayo siku ya jumanne,wakati alipokuwa akichangia hoja kuhusu mchango
wa haki za binadamu na utawala wa sheria katika kuunga mkono juhudi za
kitaifa na kimataifa kuelekea upunguzaji wa umaskini na maendeleo
endelevu.
Waziri
Migiro alikuwa mmoja wa wanajopo wanne waliojadili hoja hiyo
iliyoanzishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan
Eliasson ikiwa ni sehemu ya mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuwashirikisha wawakilishi
kutoka mataifa mbalimbali.
Pamoja
na kusisitiza haja na umuhimu wa ajenda mpya za maendeleo
kujielekeza katika kuyawezesha makundi hayo ya jamii. Waziri Migiro
ameongeza pia kwamba ni muhimu jumuiya ya kimataifa ikajikita pia
katika kupunguza pengo la uwiano wa maendeleo kati ya maeneo ya mijini
na vijijini.
“
Ni muhimu kwamba kila sehemu ya jamii ikawezeshwa ili iwe na fursa ya
kupata haki, haki ya kumiliki mali, ikiwamo haki ya kumiliki na
kurithi ardhi na haki za ajira zenye ujira sawa kwa kazi sawa”
akaeleza Migiro na kuongeza
Akasema
ili hayo na mengineyo yaweze kutekelezwa ni vema basi suala la haki
za binadamu na utawala wa sheria vikawa sehemu muhimu ya Ajenda za
Maendeleo baada ya 2015 na vilevile kwa Malengo Endelevu ya
Maendeleo.
Akizungumza
kuhusu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs),
utekelezaji wake unaelekea ukingoni.Waziri wa Sheria na Masuala ya
Katiba, anasema. Tangu kupitishwa kwa malengo hayo mwaka 2000 nchi
nyingi hasa zile zilizokuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi za
maendeleo zilijiweka sera na vipaumbele katika utekelezaji wa malengo
hayo.
“
Tumeshuhudia nguvu za pamoja katika ngazi ya kitaifa na ya kimataifa
katika kuhakikisha kwamba MDGs inakuwa kiungo cha ajenda za
maendeleo”. Na kuongeza kwamba pamoja na mafanikio ya kuridhisha
katika utekelezaji wa MDGs hizo, bado kuna mengi yakutekelezwa”.
akasisitiza Waziri.
Akizungumzi
nafasi ya Tanzania katika utekelezaji wa MDGs, Waziri amesema,
Tanzania imefanikiwa katika utekelezaji wa malengo mengi, ingawa
changamoto kubwa imebaki katika kulitafutia ufumbuzi pengo lililopo
kati ya miji na vijiji ili kuhakikisha kwamba watu wote wanakuwa na
fursa na haki sawa ya kunufaika na maendeleo endelevu.
Akasema
anauhakika kwamba nchi nyingi zinakabilia na changamoto hiyo ya
utofauti mkubwa wa kimaendeleo kati ya maeneo ya mijini na vijijini.
“Pengo
kati ya miji na vijiji ni eneo moja. lakini katika utekelezaji wa
MDGS mapengo mengine hujitokeza. Ni kwa sababu hii hapana shaka kuwa
haki za binadamu na utawala wa sheria ni viwezeshaji muhimu vya
maendeleo” akasema.
Katika
kusisitiza umuhimu wa haki za binadamu na utawala wa sheria katika
kuwapatia wananchi maendeleo endelevu. Wiziri anatoa mfano kwa kusema
ni jambo lisilokubalika kwamba karibu watu nne bilioni wanakosa haki
zitokanazo na kutoka utawala wa sheria. Huku watoto saba kati ya kumi
katika nchi zilizonyuma kimaendelo hawana vyeti vya kuzaliwa.
Waziri
Migiro anaongeza kuwa “ katika nchi nyingine uwiano kati ya jaji na
idadi ya watu unasimama katika jaji moja kwa watu milioni. Ili hali
katika nchi nyingine, watu wanaendelea kubaguliwa kwa misingi ya
makabila yao, dini au jinsia. Haya yote Mwenyekiti yanaonyesha umuhimu
wa suala la haki za binadamu na utawala wa sheria kuwa sehemu ya
maendeleo endelevu baada ya 2015”.